Wakala wa mambo ya anga wa nchini Japan wamesitisha rasmi juhudi za kuitafuta Satellite yao ya mabilioni ya fedha iliyopotea angani mwezi uliopita.

Japan-Hitomi-satellite

Mamlaka hiyo (Japan Aerospace Exploration Agency) imesema haitajaribu kurekebish kasoro zilizojitokeza katika chombo hicho kwa sababu kinaonekana kimeharibika sana hasa katika mikonga yake ya kudaka mwanga wa jua.

Kwa mara ya mwisho wanaanga hao walipokea mawasiliano kutoka katika chombo hicho tarehe 26, 2016 mwezi mmoja tu tangu kirushwe kwenda angani.

Satellite hiyo iliyopewa jina la Hitomi ilirushwa tarehe 17 February mwaka huu, ndio satellite kubwa zaidi kuwahi kutengenezwa na Japan. Ikiwa na ukubwa wa mita 14 na uzito wa tani 2.7, satellite hiyo ilitengenezwa mahususi kuchunguza mienendo ya anga hasa tabia za mashimo meusi (Black Holes) ambayo yanaonekana kuwachanganya wanasayansi wengi ulimwenguni bila majibu.

Chombo hicho kilitengenezwa maalumu kwa ajili ya kutoa miale ya X-ray itakayosaidia kuchunguza Black Holes zilizopo angani ambazo ni tishio kwa maisha ya vitu vyote vinavyopatikana angani.

Satellite hiyo ilitengenezwa kwa ushirikiano wa NASA na Japan, na baadhi ya nchi kama Canada na Uholanzi.