Tafiti zinaonyesha moja ya tano ya wateja wa benki za sasa wapo tayari kuhamia katika makampuni makubwa ya teknolojia kama Google, Amazon au Facebook kama yakiamua kuanzisha huduma za kibenki.

facebook-bank

Kupanuka kwa wigo wa huduma za kimtandao kumepelekea matumizi ya huduma za kifedha za kimtandao kuwa rahisi zaidi (online banking services) na kuwafanya watu wengi kuhamia katika huduma hizo katika kufanya manunuzi au matumizi ya kila siku ya kibenki. Swali linakuja, Je kama moja ya makmpuni haya makubwa ya kiteknolojia ya Google, Facebook au Amazoni yakaamua kuanzisha huduma zao za kibenki watu wangapi watahamia huko na kuzikacha benki zao za sasa?

Ripoti ya utafiti uliofanywa na kampuni ya Fujitsu zinaonyesha watu wengi zaidi wapo tayari kuhamia katika huduma hizo kama makampuni hayo yataamua kuleta huduma za kibenki na bima. Utafiti huu uliofanywa katika bara la Ulaya unaonyesha moja ya tano ya watu walioshiriki katika tafiti hii wapo tayari kuhamia katika huduma hizo za kibima na Kibenki kama makampuni hayo yataanzisha.

37% ya washiriki walisema wao watahamia huko kama tu mabenki yao ya sasa yatashindwa kuleta huduma bora na za kisasa. Wataalamu wa mambo ya utafiti wanasema hii itafungua milango kwa watu wengine wapya kuhamia huko.

Matokeo ya tafiti hizo yanasema pia 20% ya watu wanatumia huduma ya Bitcoin kama cryptocurrencies huku idadi kubwa ya watu wakiwa kutokea katika nchi za Ulaya Mashariki.

Je, wewe ungependa makampuni haya makubwa ya Teknolojia kuja na huduma hizi? Je, ungependa kuwa mmoja wa watumiaji wa huduma zao?