Mtaalamu wa mambo ya usalama wa kompyuta na mitandao John McAfee ameibuka na kudai amefanikiwa kuvunja kizuizi cha usalama katika jumbe za Whatsapp.

whatsapp-McAfee

John McAfee ameibuka tena mara baada ya kutulia kwa muda baada ya lile sakata la Apple na FBI na sasa amekuja na madai mapya ya kufanikiwa kuvunja vizuizi vya kiusalama vinavyomzuia mtu asiweze kuingilia mawasiliano ya jumbe fupi za maneno kati ya mtumiaji mmoja na mwingine wa huduma hiyo.

Akiwa na wadukuzi wanne wa mambo ya kiusalama wamedai kufanikiwa kuingilia mawasiliano kati ya watumiaji wawili wa mtandao huo kwa kutumia software (zanatepe) zijulikanazo kama keylogger.

Hivi karibuni WhatsApp walileta huduma mpya inayowawezesha watumiaji wa mtandao huo kuwasiliana bila ya wadukuzi kuingilia mawasiliano yao (sms encryption).

Hata hivyo madai hayo ya McAfee hayajapewa uzito na wadau wengi wa masuala ya usalama kutokana na tabia ya mtaalamu huyo kujaribu kujipatia umaarufu kwa vitu asivyoviweza. Mfano mzuri ni pale alipotangaza kuwa anaweza kudukua simu ya Farook iliyokuwa inawasumbua FBI na baadae kukiri kuwa aliongopa.